UZOEFU WA KUTOKA SEHEMU YA 1

Utangulizi

Katika nchi nyingi duniani, huweka sherehe ya kumbukumbu ya Uhuru. Sherehe hizi ni maarufu sana katika bara letu la Afrika hata katika mabara mengine ambapo nchi zao zimetawaliwa au kupitia ukoloni wa namna fulani. Hivyo katika Biblia kipo kitabu kichoeleza uhuru wa wa watu wa Mungu nacho ni kitabu cha kutoka. Kitabu cha kutoka, ni kitabu kinachoeleza Uhuru wa watu wa Mungu kutoka katika utumwa mbaya wa Mistri[i]. Kitabu cha kutoka kinaeleza watu wanaotoka kutoka kwa utumwa hadi kwenye ibada ya kweli, kutoka kumtumikia Farao hadi kumtumikia Mungu.[ii]

Uzoefu wa wana wa Israel ni uzoefu wa kila mtoto wa Mungu. Uzoefu wa kutoka hueleza namna wana wa Isarel wanavyotoka kwa ushindi na kwa nguvu ya Mungu, mkono hodari na mkono ulionyoshwa. Vivyo hivyo watoto wa Mungu wamekombolewa kutoka katika dhambi kwa mkono hodari na mkono ulionyoshwa. Yesu anasema “ Kila atendaye dhambi ni mtumwa wa dhambi” Yohana 8:32. Dhambi ndiyo utumwa mbaya kuliko utumwa wowote ule ambao umeshakuwapo. Pamoja na utumwa mbaya wa dhambi tunayo namna nyingi za utumwa unaotukabili, utumwa wa magonjwa, njaa, kukosa kazi pamoja na namna nyingine nyingi.Ellen G. White akizumza namna ya kupata uhuru wa kweli anasema “Njia pekee ambayo mwanadamu aweza kupata uhuru ni kuwa mmoja na Kristo”.[iii] Hizi zote ni namna za utumwa ambazo Mungu amekusudia kutupatia uzoefu wa kutoka.

Hali halisi

Wana wa Israel wamekaa Misri kwa muda wa miaka 430. Baada ya kupatiwa Hifadhi na ndugu yao Yusufu. Katika kitabu cha Kutoka 1:7, 12“ Na wana wa Isarael walikuwa na uzazi sana na kuongezeka mno, na kuzidi kuwa wengi, nao wakaendelea na kuongezeka nguvu; na ile nchi ilikuwa imejawa na wao. Lakini kwa Kadri walivyowatesa ndivyo walivyoongezeka na kuzidi kuenea” Pamoja na kuwa Yusufu hakuwepo lakini wao kwa kuwa lilikuwa Taifa teule liliongezeka na kukua. Mazingira na hali halisi katika kitabu cha Kutoka yalikuwa mazingira duni, mazingira ya kitumwa mazingira ya kutojulikana na mazingira ya mateso lakini katika ugumu wa mazingira yote haya bado watu wa Mungu waliongezeka.

Mungu hafungwi na mazingira wala nguvu za asili, hakuna mamlaka wala dola, inayoweza kupinga kusudi la Mungu. Upande wa Farao wakiwa na sera ya kuwaangamiza wana wa Isarel Mungu alikuwa amewapangia mipango ya wema. Yeremia 29:11 “ Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi asema Bwana, ni mawazo ya amani, wala si mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho”. Mawazo ya Mungu juu ya watoto wake siku zote ni mawazo mema, mawazo ya kutupatia amani na tumaini. Farao na serikali yake wanaweka sera za mauaji Mungu anaweka sera ya ufufuo kwa upande mwingine. Farao anaweka sera ya kuwapunguza Mungu anaweka sera ya kuwaongeza.

Mungu akasikia Kilio cha wana wa Israel

Wana wa Isarel walipolia na kuhuzunika Mungu alisikia kilio chao. Kutoka 3:7 “Bwana akasema, Hakika nimeyaona mateso ya watu wangu walioko Misri, name nimesikia kilio chao kwa sababu ya wasimamizi wao; kwa sababu ya wasimamizi wao; maana nayajua maumivu yao” Hii ni habari njema kwa wana wa Israel lakini pia ni habari njema kwa watoto wa Mungu kuwa Mungu anasikia maombi ya watoto wa Mungu. Bwana anapozungumza na Musa na kumwambia kuwa hakika, kwa maneno mengine anamwambia nimetazama kwa makini, au nimefanya upembuzi yakinifu. Katika Biblia, Mungu hakuwasikia wana wa Israel peke yo ila pia wapo watu kama Hanna naye alipolia Bwana alimsikia, Eliya alimwita Bwana, Mungu alisikia, Mwanamke aliyetokwa na damu kwa miaka 12, mwenye ukoma alipomkimbilia Yesu na kumwambia “ukitaka waweza kinitakasa”. Bradson, W hueleza kuwa, Mungu husikia nakujibu maombi. Husikia kilio cha mtoto wake aliye mhitaji anapokwenda kwake akihitaji. Si hivyo tu Mungu anaweza kusoma na kutafsiri mahitaji yasiyotamkwa kwa mdomo, yeye husoma moyoni, naye hatatupilia mbali mahitaji ya watoto wake.[iv] Akiweka msisitizo mkubwa katika hili White, E anasema kuwa Baba yetu wa mbinguni anasubiri kutumwagia wingi wa Baraka zake. Ajabu ni kwamba tunaomba kidogo sana. Mungu yuko tayari na yuko radhi kusikia ombi la dhati la kila mtoto wake, na wakati huo huo tunasita kumjulisha yeye mahitaji yetu.[v] Kama watoto wa Mungu katika uzoefu wa kutoka ni uzoefu unaotufundisha kuomba na kufanya mahitaji yetu yajulikane kwa Mungu.

Neno la Bwana linatuambia kuwa “Tazama, Mkono wa BWANA haukupunguka, hata usiweze kuokoa wala sikio lake sio zito, hata lisiweze kusikia; lakini maovu yenu yamewafarikisha ninyi na Mungu wenu, na dhambi zenu zimeuficha uso wake msiuone, hata hataki kusikia” Yeremia 59:2 Wakati mwingine maovu yetu yanafanya kilio chetu kisisikike wala mkono wa Mungu usishuke kuja kutuokoa, Nabii asema mkono wa Bwana haukupunguka, katika uzoefu wa kutoka ni uzoefu wa kuweka kando yale yote yanayoweza kufanya sauti yetu isifike kwake.

Katika uzoefu wa kutoka ni vyema kuhakikisha unamwambia Yesu mambo magumu yanayokusibu na kukutatiza. Huwezi Kumchosha, yeye hubeba malimwengu yote mabegani mwake hatashindwa kukubeba wewe na matatizo yako.[vi] Tunapolia na kuomba kwa Mungu yeye husikia

Hajiri alipolia na kuomba Mungu alisikia na kmfumbua macho

Hanna alipolia na Kumimina moyo wake kwa Bwana, Mungu alimpatia Mtoto

Yoshua alipolia na Kuomba Jua lilisimama hadi Israel waliposhinda

Hata sisi tunalia na kuomba Mungu anasikia.

 Hitimisho

Haijalishi kuwa tumekaa Misri kwa Muda mrefu au mfupi kiasi gani, Mungu amekusudia kutupatia uzoefu wa kutoka. Wakati shetani na vibaraka wake wote wamepanga mipango ya kutuangamiza na kutukomesha Mungu ameandaa mpango wa kutufufua na kutuongeza.

 

 

[i] Mafungu yaliyotumika hapa yamenukuliwa kutoka Biblia ya Kiswahili Union Version (1997) Isipokuwa imeelezwa Vinginevyo

[ii] Terence Fretheim, T Interpretation: A Bible commentary for Teaching and Preaching, (Westminster John Knox Press 2010), p 1

[iii] Ellen G. White, Desire of Ages “ The only condition upon which the freedom of man is possible is that of becoming one with Christ.

[iv] Bradson, W, Drama of Ages (Pacific Press 1950) p 234

[v] Ellen G White, Steps to Christ (Ellen G. White Estate, Inc. 2010) p 117