Yohana na Uwakili wa Talanta

Na Pr Singo, Jonas Safiel (Mchungaji wa Mtaa  wa Kigamboni)

Luka 10:54

Wanafunzi wake Yakobo na Yohana walipoona hayo, walisema ,Bwana , wataka tuagize moto ushuke kutoka mbinguni, uwaangamize;(Kama Eliya alivyofanya)?

Utangulizi

Huenda ukawa kati ya wengi wanaofikiri kuwa Yesu alichukua watu wakamilifu mno katika tabia, mwendendo, uwezo na vipawa au talanta

Katika kuangalia maisha ya Yohana utagundua kuwa Mungu amekuwa katika kazi ya kuwaita watu na kuwatengeneza kufaa kwa ajili ya kazi ya kutangaza injili. Ellen G White  anasema “Mungu  anawachukua watu jinsi walivyo, wakiwa na chembechmbe za kibinadamu katika Tabia zao, na kuwafundisha kwa ajili ya huduma yake, kama tu watajinidhamisha na kujifunza kutoka kwake. Wamechaguliwa sio kwa kuwa ni wakamilifu ila wakiwa na mapungufu, kwamba kwa kupitia uzoefu wa kweli,  na kwa kupitia neema ya Kristo, wabadilishwe kwa sura yake” (Desire of Ages 294.4)

Yesu alikuwa akiwatengeneza watu watakao chukua nuru ya injili katika ulimwengu wote. Watu hawa walikuwa wamepswa kujaa uwezo mbalimbali na karama mbalimbali zenye kufaa kwa ajili ya kazi yake. Hivyo ili kuwa na uwezo huu walihitaji kutumia wakati wa kutosha pamoja na Yesu. Ukamilifu sio kazi ya siku moja bali  ni kazi ya kila siku katika kuendelea mbele kiroho.Arthur L. Bietz anasema “Watu wanaandika vitabu, lakini Mungu anaandika watu. Kwa namna tujuavyo Yesu hakuandika kitabu, lakini aliandika watu. Nao kwa kupitia uvuvio wa Roho mtakatifu waliandika matokeo ya uzoefu wao wa kuwa pamoja Yesu Kristo” (When God met Men)

Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa Yohana alikuwa chini ya uanglalizi wa mwalimu Mkuu aliyetoka mbinguni. Yohana alikua kitalanta, kimtazamo, hata kimahusiano.

Kama Yohana; mawakili wa Mungu twapaswa kukua kuufikilia wakovu. Hatupaswi kudumaa. Kama mkulima anavyotamani mimea kukua ili kupata mavuno. Hivyo ndivyo Yesu anavyotazama mawakili wake wapate kukua na kumzalia matunda na matunda yao yapate kukaa (Yohana 15:16) .

Wito wa Yohana na Uanafunzi

Matayo hueleza mianzo ya kuitwa kwa Yohana Matayo 4:21 Yesu anamwona Yakobo mtoto wa Zebedayo pamoja na Yohana nduguye, akawaita. Biblia inasema mara wakaacha mashua zao kisha wakamfuata. Hadi Yesu anawaita, Yohana alikuwa mvuvi wa samaki. Ila Yesu akawaambia kuwa nitawafanya kuwa wavuvi wa watu.

Ellen G. white anasema “…………mwalimu mkuu alichagua watu wanyenyekevu, watu wasio na elimu ili kutangaza ukweli ambao ulikuwa utikise ulimwengu mzima. Alidhamiria kuwafundisha na kuwapatia elimu kama viongozi wa kanisa lake. Walikuwa wawe waalimu wa  wengine na kuwatuma kwa ajili ujumbe wa injili. Ili wawe na mafanikio kwenye kazi yao walikuwa wapewe uwezo wa Roho  mtakatifu. Injili isingalihubiriwa kwa nguvu za kibinadamu au kwa hekima ya kibinadamu  bali kwa nguvu ya Mungu.(Act of Apostles 17.2)

 

Yesu aliwafahamu kila mmoja wa  wanafunzi wake kwa tabia na mwenendo wao pamoja na talanta (uwezo) wao. Alimfahamu pia Yohana na mapungufu yake. Mara kadhaa Yohana anaitwa “mwana wa ngurumo” sio kuwa ndo maana jina lake. La isipokuwa ilikuwa tabia ya Yohana ya kuwa mwenye hasira, majivuno na kujikweza. Lakini Yesu alimchukua  kama alivyo ili kumweka katika shule yake ya kumfundisha tabia inayofaa kuwa mtumishi. Sio mpango mpango wa Mungu kwetu sisi kutumia uwezo Mungu aliotupatia kwa manufaa au sifa zetu bibafsi bali ni kwa ajili ya kujengana na wala sio katika kubomoa. Kuleta na wala sio kutawanya.

Yesu aliona uwezo wa kuafaa wa kazi ya injili ndani ya maisha ya Yohana. Ilimpasa tu Yohana kujisalimisha miguuni pa Yesu.Yesu anasema “ ……maana pasipo mimi hamwezi kufanya neno lolote” (Yohana 15:5) Uwezo wowote wa kutenda jambo usipounganishwa na mtoaji ambaye ni Yesu wala haitufai kitu na wala mchango wetu kwake hauna maana yeyote. Kwa kuona uwezo huu mkuu ukiokuwa ndani ya Yohana , Yesu alimpenda sana Yohana(Yohana 13:23) kwani alijua kuwa Yohana atakuwa chombo kinachofaa kwa  ajili  ya kazi nyeti ya injili. Kwa upendo huu na urafiki na Yesu Yohana aliachwa na Mama wa Yesu.(Yohana 19:26)

Yohana alikuwa na mengi ya kujifunza kutoka kwa Yesu. Alikuwa ajifunze huruma na upendo. Mara nyingine alikuwa akitumia uwezo kwa matumizi mabaya. Katika fungu letu tangulizi anaonekana kutaka kuwaangamiza woote ambao hawakumkaribisha Yesu huko samaria. Hivyo mwalimu mkuu Yesu akamkumbusha kuwa kazi yao sio kuangamiza bali kuokoa na kuponya. Yohana alikukuwa akipitia kipindi cha mpito kutoka alipokuwa hadi kufikia kiwango alichokitaka Bwana Yesu.

Kama Mwalimu Mkuu kutoka mbinguni Yesu alifundisha wanafunzi 12 wote walifaulu kwa daraja la kwanza (Division 1) hata Yohana aliyekuwa mwenye hasira na majivuno alifaulu. Ila Yuda alipata daraja la 0 (Zero). Sio kwamba Yuda hakuwa na uwezo, la ila hakukubali kubadilika, pamoja na uwezo(talanta) alizokuwa nazo; hakukubali maelekezo ya Mwalimu.

Kufaa kwa Yohana

Yohana ambaye maana ya Jina hilo ni “neema ya Mungu” anaonekana kunyenyekezwa sana baada ya Bwana wake kupaa. Baada ya Yesu kurudi kwa Baba yake  Yohana anaonekana kutumia talanta mabalimbali Mungu alizoweka kwake sio kwa ajili yake kama ilivyokuwa awali bali kwa ajili ya Bwana wake  aliye mwagiza akisema “Basi, enendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi mkiwabatiza kwa jina la Baba , na Mwana, na Roho mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja  siku zote, hata ukamilifu wa dahari” Matayo 28:19,20.

Baada ya kupaa kwa Yesu Yohana anaonekana kusheheni talanta mbalimbali kwa ajili ya huduma na ukuaji wa kanisa la awali.

Ø       Talanta ya Kuhubiri: Yohana anaonekana akihubiri habari za Yesu sio kwa hasira na majivuno bali kwa ujasiri mkuu sana na wengi wakimwamini Bwana Yesu. Matendo 3,4

Ø       Talanta ya Kuponya: Petro na Yohana wanakwea kwenda hekaluni kusali wanamwona ombaomba kiwete amekaa akitaraji kupata kitu kutoka kwao nao wanamwambia Kwa jina la Yesu Kristo simama uende. Matendo 4

Ø       Talanta ya ujasiri: Yohana pia anatumia uwezo wake wa kujiamini kumshuhudia Yesu. Matendo 4:13

Ø       Talanta ya Uinjilisti wa mahali papya: Makanisa ya Simrna,Pergamo, Sarid, Filadelfia,Laodekia na Thiatira. Haya  ni makanisa yaliyofunguliwa na Yohana. (Fox’s Books of Martyrs Chapter 1)

Ø       Talanta ya Uandishi: Yohana anafanya kazi kama mwandishi akiandika habari za Bwana wake Yesu.

o       Yohana  anaandika Injili ya Yohana – kuelezea habari za mwokozi na Bwana wake Yesu hii ni baada ya kutoka Patmo

o       Akiwa katika kisiwa cha patmo baada ya kuwekwa kwenye pipa linalochemka mafuta bila ya kuiva. Yohana akiwa hapa katika kisiwa hiki anaandika kitabu cha ufunuo chenye unabii mkuu wa Biblia  -  Pia ni wakati Yohana akiwa hapa Patmo anapoonyeshwa mji wa Yerusalemu ambapo mimi na wewe tutakaa milele.

o       Baada ya Kutolewa Patmo na Mfalme Nerva aliyechukua nafasi ya Mfalme Domitian. Yohana anaandika Nyaraka nne. Akieleza uzoefu wake wa ukristo. Anaandika Waraka wa I ,II ,III, IV kwa watu woote.

 

MUHIMU: Yohana ni mwanafunzi pekee kati ya wanafunzi wa Yesu amabaye hakuuawa kwa ukatili ila maisha yake yaliisha kwa amani. Pamoja na maisha yake kuishia kwa amani, ni maisha yaliyokuwa yamejawa na majaribu na mateso makubwa aliyosinda kwa uwezo mkuu wa Yesu.

Baada ya kukaa chini ya Miguu ya Yesu, Yohana anatumia   talanta zake zote (UWEZO) kwa ajili ya utukufu wa Mungu. Kabla ya hapo alitumia uwezo wake kwa ajili ya manufaa yake.

KUMBUKA “Kila talanta yaweza kutumika kumtukuza mwenye kuitumia au kumtukuza yeye aliyeitoa” (Seventh Day Adventists  Believe, Second Edition p 303.4)

Je uwezo wako unautumia kwa ajili ya nani?

Je uwezo wako wa kuimba? Unautumia kwa manufaa ya nani?

Uwezo wako wa kuhubiri ? Unahubiri kwa kumwinua nani: wewe mwenyewe au Yesu?

Habari gani Uwezo wako wa kufundisha? Unafundisha habari za nani?

Kama Yohana  tutumie talanta zetu zote kwa utukufu wa Mungu

Bwana awabariki Sana.